HAKUNA Mtanzania asiyetambua hivi leo kuwa Tanzania iliyokuwa mbele katika siasa za mageuzi na kukubali ujio wa demokrasia inaachwa nyuma na Kenya nchi iliyochelewa sana kukubali demokrasia.
Kiuchumi, hali kadhalika, Kenya sasa ni tishio kubwa kwa Tanzania kuliko nchi nyingine Afrika Mashariki na kati. Ukichanganya uchumi imara wa Kenya na kasi yao ya mageuzi ni dhahiri kuwa Tanzania itakuwa na wakati mgumu sana kama itaendelea kudengua katika kukubali mabadiliko yenye mapana, marefu na kina cha kutosha kuwa changamoto ya maendeleo ya aina mbalimbali.
Ni katika muktadha huu ndio tunajitoa hadharani kama wanachama na wapenzi wa CCM kukipa changamoto chama chetu na Mwenyekiti wetu mpenzi, Jakaya Mrisho Kikwete kuchangamkia mara moja suala la Tanzania kuwa na Katiba mpya mapema iwezekanavyo.