Wednesday, March 30, 2011

Maudhui na misingi ya Katiba Mpya:

Kijumla katiba lazima iwe ya watu na itakayowatumikia watu na matakwa yao na sio kuwa silaha ya kuwakandamiza, kuwanyanyasa na kuwapora utawala wa nchi yao

wazawa na watu wa nchi hii kwa ujumla.

Huu ni uwanja mpana na maoni yangu kijuujuu ni kwamba:
i. Katiba Ihakikishe ina vifungu toshelevu kuhusu haki za mtu (individual) ili jiji na miji yetu isiwe inatumia askari kuwafukuza machinga, mama ntilie na watu

wengine wanaotafuta riziki zao bila kueleweka watu hao wana haki gani. Yaani, mtu akifanya kosa ijulikane ni kosa moja kwa moja toka ndani ya katiba na sheria za

nchi. Na mtu akipewa upendeleo katiba ifichue kuna upendeleo waziwazi. Tusivumilie katu tabia ya kujengwa Vijiwe vya kina CCM mitaani na pale wakaruhusiwa

kuvunja sheria eti kwa kuwa wanaishabikia na 'kuitetea' CCM !

ii. Katiba lazima iwe very specific kwenye hali inayojitokeza nchini ambayo baadhi ya polisi na mahakimu wanaonekana kupiga bei au kuuza na kununua haki

za watu!

iii. Mamlaka ya rais yapunguzwe kwa kiasi kikubwa na ikiwezekana asilindwe pale atakapoonekana na viongozi wenzake kuwa kavunja sheria na katiba ya nchi.

iv. Jaji Mkuu atokane na majaji kadhaa watakaopendekezwa bungeni na kisha kuchaguliwa na bunge.

v. Kamanda mkuu wa polisi atokane na majaji kadhaa watakaopendekezwa bungeni na kisha kuchaguliwa na bunge.

vi. Mwanasheria Mkuu atokane na majaji kadhaa watakaopendekezwa bungeni na kisha kuchaguliwa na bunge.

vii. Katiba ifafanue maana ya Uchochezi na Uhaini katika mazingira ya mfumo wa vyama vingi na kila kitu kiwe bayana na kueleweka vyema na kukubalika na

wote. Tusikubali Watanzania fulani kuwaita wenzao wahaini na wachochezi kwa sababu Watanzania wenzao wamegundua wao ni wezi na mafisadi.

viii. Benki Kuu na Hazina lazima ishurutishwe na Katiba kutenga asilimia fulani katika kusaidia masikini na kuendeleza wazawa.

ix. Wakuu wa mikoa wasiteuliwe na rais bali wachaguliwe na wakazi wa mikoa husika ili kuwawajibisha ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

x. Mikoa iwe na Gavana au Waziri wake mkuu na baraza lake la mawaziri na wa wawakilishi wa mikoani watakaounda bunge la mkoa wakitokea kwenye watu wa

kuchaguliwa na wale wa kuwakilisha maslahi ya makundi mbalimbali katika jamii. Hili litaifanya mikoa kushindana katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi na hivyo

kuendelea kwa haraka zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

xi. Ruksa kwa vyama vya kisiasa kuungana kama ilivyo rahisi kwa watu wa kawaida kufunga ndoa wakati wowote wanapotaka.

xii. Kutoruhusu udikteta katika kundi au chama chochote cha kisiasa au kijamii na kadhalika.

xiii. Mkuu wa TUC (Tanzania University Commision) kupewa kazi na bunge na wakuu wa vyuo vikuu vyote kutathminiwa na kuchaguliwa na TUC!

xiv. Katika migodi na madini katiba itaje wazi utaratibu wa kumiliki, kukodi, kuchimba, kutengeneza vitu vinavyotokana na madini na kuviuza vitu hivyo kwa

manufaa ya wananchi. Lazima pia mipango iwepo ya kuiwezesha nchi hii kwanza kununua na kutengeneza mitambo muhimu kwa sekta husika ili wananchi wafaidi zaidi

mali asili yao. Taratibu hizo ni pamoja na kutaja mrabaha unaokubalika; mtawanyo wa umiliki kwa nchi za Mashariki na Marekani ya Kusini zaidi kuliko zile zilizozoeleka

za Magharibi.

Xv. Katika Umeme lazima katiba ieleze waziwazi aina ya umeme salama na bora kwa nchi na watu wasiwe wanaropoka ropoka tu kuhusu vitu kama umeme wa

nyuklia kwa nchi ambayo imeshindwa kusimamia vyema vitu vya kawaida; ikaja tokea viongozi wetu wanashawishika kuzalisha umeme huo hatari kwa maafa ya vizazi

vijanvyo.

xvi. Kuhusu maji ni lazima katiba iwe chimbuko la sheria ambazo zitakuwa kali na zisizo na huruma kuhusu kutunza vyanzo vya maji na vile vile kuhamasisha

ubunifu na matumizi mazuri ya maji toka kwenye maziwa yanayotuzunguka; bahari, mitoni, ardhini na yale yanayoletwa na mvua.


xvii. Kuhusu Utalii ni lazima katiba ioneshe waziwazi jinsi ambavyo wanavijiji na wanajamii mbalimbali bara na pwani watakavyonufaika na utalii badalal ya utalii

kunufaisha matajiri wachache wa nje na ndani. Ni lazima serikali iainishe mipango na mikakati ya wananchi pwani na bara kutumia ardhi, bahari na vivutio walivyo navyo

kama mtaji wao na hivyo kuhesabika kithamani na kifedha na kukubaliwa na wawekezaji kama uwekezaji wa thamani, halali na unaokubalika katika uendeshaji utalii na

mambo kama hayo.

xviii. Kuhusu viwanda ni muhimu katiba ichambue ndani-nje aina ya viwanda vinavyohitajika na jinsi tunavyoweza kuongeza thamani ya mazao, bidhaa, madini na

mali asili nyingine zetu ili tunufaike zaidi kiuchumi kuliko kunufaisha watu wa nje. Ni lazima kujipanga pia kikatiba na kuona kuwa tunazalisha mashine-mama na

mitambo-mama yote tunayoweza ili uendelezaji sekta ya viwanda uwe rahisi. Katika miaka hii ambayo wahandisi na wataalamu mbalimbali Ulaya, Asia na kwingineko

hawana kazi ni muhimu katiba ikaribishe watu kama hao ili kuongeza nguvu zetu kiteknolojia na kifikra na kiubunifu.

xix. Katika kilimo katiba iweke misingi imara ya ujio wa mapinduzi ya kilimo na pia uundaji wa matrekta madogo kwa makubwa papa hapa nchini ili kuhakikisha

kwamba kilimo chetu hakitegemei mitambo na zana kutoka nje. Na zaidi ya hapo tunakuwa na nafasi nzuri ya kuuza kwingineko zana bora na rahisi za kilimo kwenye

nchi zinazotuzunguka. Ni muhimu katiba ifahamishe umma jinsi ambavyo maendeleo ya kilimo yatakavyosababisha idadi ya wakulima kupungua na watu wengi zaidi

kutegemea ajira nje ya kilimo na jinsi ya kujiandaa kwa majaliwa hayo.

xx. Katiba iamue kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na wajumbe watakavyostahili kupatikana.

xxi. Katiba iweke miiko kwa jeshi, polisi, usalama wa taifa kuingiliwa au kuingizwa katika masuala ya kisiasa ikiwemo uchaguzi mkuu.

xxii. Katiba isaidie pia kufafanua haki na fidia za wale wanaolazimika kuachia kitu au vitu fulani, wanaoharibikiwa mali zao kutokana na uzembe wa mtu au shirika

fulani; wanaopata ajali au kupoteza kitu fulani. Fidia hiyo iwe kiasi kinachompa mtu unafuu wa kweli na anayeadhibiwa kuona uzito wa makosa zake na kuwa kama dawa

ya tabia zisizokubalika. Katika suala hili la fidia kusiwe na kinga kwa mtu au taasisi au idara yoyote ya serikali ili kuzuia uzembe na upuuzi katika maamuzi yetu wote.


xxiii. Ardhi katika katiba iendelee kuwa ni mali ya taifa. Hata hivyo, wananchi wote wawe na cheti cha umilikaji na wageni/wawekezaji waruhusiwe kukodisha ardhi

kwa miaka 33, 66 na 99 lakini wasiwe na ruksa ya kuuza. Yeyote anayefanya ujanja ashtakiwe, anyang'anywe na afukuzwe nchini.
Katiba iruhusu matumizi ya ardhi katika miji yetu kuboreshwa (urban upgrading), ikiwa ni pamoja na kuondoa baadhi ya mitaa ili kuwe na bustani na viwanja

vya kupumzika na michezo kwa watoto na vijana. Maeneo ya umma yawe ni kwa ajili ya matumzi kwa umma na vinginevyo iwe ni kosa na uhalifu mkubwa nchini.

xxiv. Katika katiba haki ya Mtanzania kuwa na nyumba ibainishwe waziwazi. Na mchango wa serikali, wizara na taasisi zake mbalimbali katika hili ufahamike. Pawe

na mifuko, benki na vyama vya kusaidia ujenzi wa nyumba kwa gharama nafuu. Ifikie wakati ambapo ni Watanzania wachache watakuwa wakizungumza mambo ya

ujenzi wa nyumba au kwenda saiti na vitu kama hivyo kwa sababu kutakuwa na makazi ya kutosha katika maeneo mbalimbali ya nchi na kazi kubwa itakayobakia ni

ukarabati na uboreshwaji.

xxv. Katiba iwe kichocheo cha madaktari, manesi, wahadhiri, walimu na wale wote ambao wanasoma kwa muda mrefu na kufanya kazi katika mazingira magumu

kulipwa vizuri kuliko wanasiasa. Tabia ya kuwalipa wanasiasa mishahara mizuri kuliko wale wanaojikunya kufanya kazi ngumu na muhimu nchini ndiyo iliyotufikisha hapa

tulipo leo.


xxvi. Katiba iweke wazi kiasi cha GDP kitakachotumika katika utafiti na maendeleo kwenye maeneo mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya nchi kitaalamu na

kitaaluma.

xxvii. Katiba iwe kichocheo cha matumizi ya vifaa na zana zisizo chakavu na hususan vile vya uchukuzi na usafiri. Ijulikane kabisa basi linatakiwa lisizidi miaka

mingapi kuwa barabarani, ndege na helikopta hewani miaka mingapi na meli baharini, mitoni na maziwani nazo zisiabiri zaidi ya miaka mingapi.

xxviii. Ni lazima pia katiba ianishe kuwa ni jukumu la kiongozi au viongozi wa juu kabisa kuhakikisha kuwa nchi yetu ina hali ya usafi na utunzaji mazingira wa

kuridhisha. Na kuwa kigezo kimoja cha uongozi bora kiwe ni usafi wa nchi na miji yake.

xxix. Sehemu zote za huduma ikiwemo mahoteli, maduka, mabaa lazima yawekewe katika katiba na sheria za nchi nguvu ya kikatiba kwamba huduma

zinazotolewa lazima ziendane na kule tunakotaka kuipeleka nchi, nikiwa na maana, lazima tufanane fanane na Uchina, Uarabuni, Ulaya, Marekani na sio vinginevyo. Hili

litasaidia sana nchi kuuzika kirahisi kama eneopendwa la watalii duniani. Hivi sasa tunashika nafasi ya nane duniani lakini hatua hizo zikichukuliwa upo uwezekano wa

kuwa 4.



XXXXXXXXX

kitilam@udsm.ac.tz