MCHAKATO halali wa katiba unastahili kufuata utaratibu kama huu hapa chini au unaokaribia kufanana nao (kwa kuzingatia kwamba ridhaa inaweza kutoka kwa kiongozi lakini maamuzi yanatoka kwa wawakilshi halali wa wananchi ndani na nje ya bunge), na unaozingatia kuwa washika mamlaka na madaraka ya nchi ni watu na sio serikali na viongozi wake (maana hawa ni vibarua tu):
1. Kiongozi wa serikali iliyopo madarakani (kwa kuzingatia nchi inafuata mfumo wa vyama vingi), analiandikia bunge kuwa wanaowawakilisha wanataka katiba mpya, hivyo bunge lishirikiane na wawakilishi wengine wa wananchi kupitia vyama vyao mbalimbali, ikiwemo vya wafanyaazi, kitaaluma, kijamii na kadhalika kuandaa muswaada wenye ridhaa ya wananchi kuanza mchakato wa kutafuta katiba mpya. Hatua hii ni muhimu kwani inadhihirisha kuwa rais si mfalme, bali ni mwajiriwa wa wananchi;
2. Bunge linawaarifu wananchi juu ya kukubaliwa kwa madai yao ya kupata katiba mpya na kuwaomba wasio na uwakilishi wa aina nyingine nje ya bunge kufanza haraka ya kuwatafuta wawakilishi wao ili washiriki katika Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya;
3. Wabunge wanarudi kwenye majimbo yao na kuwasaidia wananchi wao kupata wawakilishi katika kila eneo ikiwemo yale ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kiimani;
4. Wananchi wanapendekeza kwa ushauri wa bunge idadi ya wajumbe na makundi maslahi na maalum yatakayo wakilishwa, katika Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya;
5. Waliochaguliwa wanaketi kama wajumbe wa Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya kuchagua kamati mbalimbali mojawapo ikiwa ile ya kuandika muswaada wa kisheria kuhusiana na mchakato wa katiba mpya, tofauti na ilivyofanyika kwa kutokea ofisi ya rais na watumishi wa chama tawala nchini;
6. Muswaada unaidhinishwa na asilimia ya wajumbe iliyokubalika awali na kuwasilishwa kwa viongozi na washika dau mbalimbali kama taarifa na vilevile kwa nyongeza au ukinzani ili urekebishwa na kuimarishwa zaidi kwa faida ya walio wengi;
7. Mgawanyo wa kazi katika Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya unafanyika na kazi mbalimbali kuhusiana na kuhamasihwa na kuelimishwa wananchi; kuandka rasimu mbalimbali; kujifunza toka nchi nyingine na kukusanya mawazo na fikra za wananchi ndani na nje ya nchi zinaanza;
8. Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya linapaswa kuwa na vikao kadhaa vya kutathmini kazi na ubora wa kazi iliyofanyika katika hatua mbalimbali na wakati huohuo kuwa na uwezo wa kisheria wa kuamrisha yanayostahili kufanyika kwa manufaa na faida ya nchi, sheria, usalama na haki za wananchi/binadamu kufanyika bila ya kusubiri mchakato kukamilika. Vikao hivi vitakuwa wazi na huru na kuhudhuriwa na yeyote yule anayetaka ili kukamilisha dhana ya wananchi kudhibiti mchakato mzima toka mwanzo mpaka mwisho;
9. Ili kuliepusha taifa na mzigo wa kubeba gharama kubwa katika zoezi la kupata katiba mpya Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya litapaswa kuweka muda wa mwisho wa kufanya kila jambo na gharama zitakazoendana na kila shughuli inayopaswa kufanyika;
10. Baraza lina haki ya kukataa na kubatilisha tamko, sheria au hatua yoyote ile ambayo italifanya zoezi la kuandika katiba mpya kuwa gumu, la kiujanjaujanja, kitu kisicho wazi au lenye mizengwe kwa faida ya mtu au chama fulani;
11. Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya lina haki ya kuomba wataalamu wa mambo ya sheria toka ndani na nje ya nchi kuajiriwa ili kurahisisha na kufanikisha zoezi hilo kama lilivyopangwa;
12. Baraza la Kitaifa la Kuandika Katiba Mpya litakuwa huru kutangaza mahala linapokwama, nani analikwamisha na aidha kuomba ridhaa toka kwa wananchi kwa muda wa kufanya kazi zake ili zikamilike vizuri kama ilivyopangwa toka mwanzo.
No comments:
Post a Comment