WAKATI tayari wabunge wanashinikizwa kuusoma mswaada wa katiba mpya kwa mara ya pili badala ya kusomwa mara ya kwanza, ninachukua fursa hii kuwaasa viongozi na wabunge wetu kwamba kitendo cha kuusoma mswaada huu kama unaosomwa mara ya pili haitakuwa tofauti na wao kuipindua katiba ya nchi na kosa hilo ni sawa sawa na mapinduzi ya kijeshi, tofauti ikiwa yale ya kijeshi watu wengi watakufa siku hiyo hiyo, wakati haya ya kikatiba Watanzania wote watakuwa wanauawa taratibu na kimya kimya.
Watanzania wana haki kwa kutumia wawakilishi wao wa kweli na halali kuhusiana na suala la katiba na sio wanafiki na vibarakala wa wale walioko madarakani, kuchukua hatua zote za kisheria ni kiharakati ili 'wanaoazimia kuipindua' katiba kinyume cha sheria wanachukuliwa hatua zinazostahili. Na sio tu serikali imeamua kuipindua katiba, bali inawaziba mdomo na masikio wananchi ili wasijue kinachofanyika kwa kuwatumia wale waliochaguliwa kulinda haki na maslahi ya watawala na sio ya watawaliwa!
Aidha, damu, dhiki na machungu yoyote yatakayosababishwa na kuusoma na kuupitisha mswadaa huu, laana yake iwaangukie viongozi wa Tanzania wa zamani na wa sasa.
Tunajua ugumu wa viongozi wa Afrika na hasa hawa wetu wa Tanzania kusalimu amri. Inatisha pale viongozi hao tena wanaposemekana ni wale wanaosalmi amri kwa Mwenyezi Mungu, lakini labda si hawa wa sasa...na kama wanalaghaiwa na wale wanaowashauri kwa sababu binafsi za washauri hao, basi huu ni wakati muafaka wa hususan rais, kusalimu amri na kuwarudishia Watanzania haki yao ya kikatiba ya kuwa ndio wenye mamlaka na madaraka ya juu kabisa kwenye suala kama hili na sio yeye rais. Anachoshauriwa kukifanya rais kwa hivi sasa ni sawa na 'kuwapindua Watanzania' kwa kuipindua katiba yao iliyopo hivi sasa ambayo ndiyo inayosema wao ndio wenye sauti ya mwisho juu ya katiba na sio rais.
Kwa kuzingatia hayo hapo juu, ni muhimu awali ya yote kuweka jambo moja muhimu kuliko yote sawa hapa. Je, ni rais au ni wananchi wenye haki ya kusimamia mchakato wa katiba mpya ? Je, rais si kiongozi wa seriikali taasisi ambayo ni mmoja wa wadau katika suala hili la katiba? Na rais huyo huyo sio mwenyekiti wa chama tawala ambacho ni mmoja wa wadau katika suala hili la katiba? Katika hali kama hii haki na uadilifu uko wapi? Ni katiba gani inayomruhusu rais kuwapora wananchi haki yao ya kuwa ndio walio na mamlaka na madaraka ya juu na ya mwisho kwenye masuala kama haya?
Kuna mambo kadhaa ambayo ninafikiri ni muhimu
kuwekwa wazi na ikiwezekana kutekelezwa hata kabla ya Tanzania kuwa na katiba mpya.
1. Mosi ni ufafanuzi wa nani ndiye mwenye sauti na maamuzi kuhusu mchakato wa katiba mpya kwa mujibu wa katiba tuliyonayo, yaani, ni nani kati ya wananchi kupitia chombo au vyombo vyao halali vya uwakilishi vilivyopo au kitakachoundwa au ni serikali na kiongozi wake. Utata unakuja pale tunapobaini kwamba serikali nayo pia ni mdau katika mchakato huu. Na kwamba si haki kwa chama au serikali kujipa mamlaka au madaraka ambayo hawastahili kuwa nayo, kwani huko ni sawa na kupora mamlaka ya wananchi na kufanya mapinduzi ya kikatiba bila kutumia silaha.
2. Haki ya Kuandamana na Maandamano. Tofauti na katiba ya sasa inavyoruhusu, utawala wa sasa, unadai kwamba watu hawana uhuru wa kuandamana na kufanya maandamano. Pamoja na kuwatia ulemavu wa maisha baadhi ya Watanzania wasio na kosa, usalama wa taifa na vyombo vya dola hususan FFU, vinatumika kuvuruga amani na kuharibu mali za Watanznia. Kazi ya usalama wa taifa na vyombo vya dola si kuzuia maandamano na mikutano bali kuweka taratibu za kuhakikisha wanaofanya mikutano na maandamano hayo wana ulinzi na usalama wa kutosha.
3. Haki ya kukutana na kufanya mikutano. Ilivyo hivi sasa kama hapo juu inaonekana Watanzania hawana haki ya kukutana na kufanya mikutano inayohusu maisha na maendeleo yao na mitaa na vijiji vyao ila pale wanaporuhusiwa na chama tawala kupitia serikali yake iliyoko madarakani.Kazi ya usalama wa taifa na vyombo vya dola si kuzuia maandamano na mikutano bali kuweka taratibu za kuhakikisha wanaofanya mikutano na maandamano hayo wana ulinzi na usalama wa kutosha.
4. Mikoa na haki za wakazi wa mkoa. Hali ilivyo sasa chama tawala na wale wanaoteuliwa kuwa viongozi wa mikoa wanachaguliwa sio kwa uwezo wao wa kimenejimneti na kuchangia maendeleo ya wakazi wa mkoa husika bali kwa sababu za kisiasa. Ni mfumo wa kikoloni ambao mkoloni mkuu anachagua wakoloni wa kumasaidia kuidhulumu na kuinyonya mkoa husika. Tz. kwa mfano mikoa ya Mwanza na Arusha hivi leo. Mikoa inastahili kutawaliwa na chama ambacho kina wabunge na madiwani wengi katika mkoa husika na sio vinginevyo. Aidha, kukidhi changamoto za kimaendeleo zilizopo wakati umefika kwa mkoa kuwa na Waziri wake mkuu na baraza lake la mawaziri wa mkoa husika ili kuimarisha uhuru, umoja, haki na kuharakisha maendeleo ya mkoa husika.
5. Endapo kiongozi anatoa AHADI na anashindwa kuzitekeleza nini kifanyike dhidi yake na wanaohusika kwa ujumla?
6. Nini liwe jukumu la serikali na wanasiasa kuhusu mustakabali wa vijana wasio na ajira, wamachinga na waendesha biashara ndogondogo.
7. Haki ya vyama kuungana. Mpaka sasa haieleweki kwanini kuna ugumu kwa vyama vya kisiasa kuungana ili kupunguza utitiri wa vyama nchini ambao hausaidii kuimarisha mfumo wa vyama vingi nchini bali kuudhoofisha zaidi na zaidi.
8. Haki ya Mgombea huru nchini. Mpaka sasa sheria imepindwa na katiba imepinduliwa kinyemela kwa kumnyima haki Mtanzania anayetaka kugombea uchaguzi bila kufungamana na chama chochote cha kisiasa.
9. Apartheid ya viongozi kutibiwa nchi za nje wakati walalahoi wanakufa kwa kukosa fedha za kuchangia katika zahanati na mahospitali sehemu mbalimbali nchini iendelee au ife kwa kuwa na hospitali bora zaidi nchini na madakta wasio na kazi kwenye nchi zenye matatizo ya kiuchumi hivi leo duniani.
10. Nini iwe nafasi ya upinzani katika uongozi wa nchi, mikoa, wilaya na majimbo? Na je tutarahisishaje vyama mbadala kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika sehemu mbalimbali nchini.
11. Vyama viendeshwe vipi ili vipate mapato halali na sio kutegemea hazina ya serikali au kupata fedha kupitia njia ambazo zitahatarisha uhuru na utu wetu.
12. Vipi vinastahili kuwa vyombo vya habari vya wananchi na vipi vya serikali na chama tawala. Mkurugenzi achaguliwe vipi na nani? Uhuru wa vyombo hivyo utahakikishwaje?
13. Nini iwe kazi za majeshi yetu wakati wa amani? Yatashirikishwaje katika uzalishaji mali, huduma za jamii, biashara, uchimbaji madini ili kuhakikisha rasilimali za Watanzania hazipewi sawa na bure kwa wageni eti tu kwa sababu hatuna utaalamu na mitambo ya kufanya shughuli fulani?
14. Nini yawe majukumu ya usalama wa taifa ili uwe na tija zaidi katika maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia ya Watanzania kuliko ilivyo sasa. Na je ni sahihi usalama wa taifa kuchunguza viongozi wa zamani au wa upinzani kikatiba na kisheria?
15. Je, mamlaka ya Rais kuteua watu kama wakuu wa polisi, wakuu wa mikoa, wakuu wa Wilaya, majaji, mahakimu, wabunge wasiochaguliwa ni jambo zuri na linaloimarisha demokrasia au ni baya na linalodhoofisha uhuru, haki za binaadamu na demokrasia. Nini kifanyike kumaliza utata huu?
16. Je, Soko huru linastahili kuingiliwa na viongozi wa serikali ili kutafuta umaarufu wa bei rahisi? Nini kifanyike kama tumeshakubali kuwa nchi ya kibepari na soko huru. Nchi ifuate mfumo gani wa kisiasa bora kuliko ubepari na ukomunisti kesho na keshokutwa? Nini kimilikiwe na wageni na watu binafsi au wanajamii husika au serikali au ubia wa aina hii au ule?
17. Je, tunahitaji kikomo cha safari za nje ambazo kiongozi aliyeko madarakani anaweza kuzifanya katika kipindi chake cha miaka 5?
18. Je, ni magari ya aina gani na gharama gani wanastahili kuwa nayo viongozi wa serikali na wabunge na watumishi wa umma?
19. Ni vipi maji ya mito, maziwa, bahari, ardhini na mvua yanaweza kupatikana na kuhakikisha upatikanji wa maji safi kwa Watanzania sehemu zote za nchi na wakati wote?
20. Je, ni wanasiasa au watu wenye utaalamu fulani, k.m. walimu, wahadhiri na madaktari ndio wanaostahili kulipwa vizuri zaidi? Na kwanini mwanasiasa asilipwe kutokana na tarafu au kazi aliyoisomea na cheo anachostahili kuwa nacho wakati huu?
KIMSINGI, hayo hapo juu ni machache tu katika kero, vilio, matamanio, ndoto na matarajio ya Watanzania na hususan vijana ambao ndio wazazi na wenye nchi wa kesho kuhusu jinsi ambavyo wangelipenga kuona suala hili la katiba likishughulikiwa kama inavyostahili na sio kwa kutumia ujanja, maguvu, mabavu, uzaini, uzandiki, ubabe na uhuni huku wanaofanya hivi wakijua fika kwamba njia wanayotupeleka ni ya shari na siyo ya kheri!!!
Kama Rais, waziri mkuu, mawaziri, wabunge, jaji mkuu, mwanasheria mkuu na washauri wengine wa waheshimiwa wana nafasi ya kuonesha hekima na busara basi ni leo Jumatatu, tarehe 14, Novemba 2011 ni KUSALIMU AMRI NA KURUHUSU MSWAADA HUU USOMWE MARA YA KWANZA NA SIYO YA PILI!!!
No comments:
Post a Comment