Monday, May 2, 2011

Yamahitajika Mapinduzi ya Uongozi ngazi za chini

KUNA tabia iliyojengeka miongoni mwa Watanzania kwa baadhi yao kujiona bora na hivyo kuona kwamba nafasi au vyeo vya chini katika uongozi sio laiki yao. Kwa sababu wenzetu hao wanajiona wamesoma sana, matajiri sana au wana vyeo vikubwa sana basi wanawaachia watu wasiosoma, masikini na wanyonge nafasi za uongozi katika ngazi za chini kama vile usimamizi wa nyumba kumi, ukatibu kata, uenyekiti wa mitaa na udiwani. Wao wote wanakimbilia kuwa wabunge, wawakilishi na maraisi japo wanajua fika nafasi hizo ni chache mno na kwamba uongozi si lazima uwe mbunge au waziri au rais wa nchi. Chukulia mfano wa Zanzibar kuna wagombea wengi tu ambao wangelifaa kuwa wakuu wa mikoa na wakaleta mabadiliko ya kweli katika jamii lakini hawataki nafasi hiyo ila wanataka tu urais. Kuna nini Ikulu na kwenye bunge ndugu zetu ? Kwanini vipaji hivyo msivitumie kwenye ngazi ya mkoa na wilaya ? Au mwadhani nafasi zimejaa ? Matokeo yake ni kwamba taifa zima katika ngazi za chini halina viongozi ambao wanajua menejimenti, uongozi (leadership), utawala (governance) achilia mambo kama uchumi, sosholojia, saikolojia, usimamizi wa bajeti na fedha, kompyuta na teknohama, teknolojia nyingine za miaka hii na mlolongo wa mengi mengineyo yanayohitajika katika dunia ya siku hizi ili kuleta mabadiliko ya kina na kimsingi katika jamii inayoongozwa.

Funzo ambalo ningelipenda lijulikane asubuhi na mapema na dhamira kuu ya insha hii ni kwamba bila kuwa na viongozi walioelimika, walioridhikia kimaisha na wanaojua kutofautisha kati ya kutumiwa na viongozi na kuongoza wenyewe nchi hii haitaondokana na umasikini wa kutupwa kwa miaka mingi ijayo.

Kwa maneno mengine, mapinduzi ya kweli ya kiungozi yatakuja tu pale tutakapokuwa na viongozi wa ngazi za chini wanaojua uongozi, uchumi, nadharia tofauti za njia, mbinu, mikakati ya maendeleo na elimu zinazoendana na masuala kama hayo. Hawa watakuwa ni viongozi wanaoweza kuunda baraza la mawaziri la mkoa na ambao wanaweza wakahoji maamuzi yanayofanywa na bunge la taifa na baraza la mawaziri la taifa kwa kuwa wana elimu sawa na walioko juu, ingawa wao zaidi ni katika lugha mama ya taifa, Kiswahili.

Isitoshe uongozi wa namna hii ukipatikana katika ngazi ya chini kabisa itakuwa ni rahisi kutathmini viongozi na kuwapa dhamana kubwa zaidi kulingana na mafanikio yao katika ngazi za chini.

Chini ya Uongozi wa kijamaa Watanzania wengi waliokuwa na elimu, vyeo na mali walikataa katakata kugombea nafasi za ujumbe wa nyumba kumi,udiwani na uongozi wa mitaa. Ikawa ni kawaida kwa nafasi hizo kuchukuliwa na watu wasiokuwa na elimu au wenye elimu ndogo sana; wasiowahi kushika cheo chochote na waliokuwa wanaongoza kwa umasikini na hali ngumu ya maisha katika mitaa yao.

Hali hiyo ukienda leo kwenye mikoa mbalimbali na hasa huko vijijini bado ipo na inaendelea. Swali la kujiuliza ni kwamba ikiwa familia, mitaa na vijiji ndio msingi au matofali ya msingi ya taifa leltu hivi kweli tunaweza kujenga taifa lililo imara kisiasa na madhubuti kiuchumi, kijamii, kitekonoojia na kijeshi endapo uongozi wake unashikwa na watu sampuli hii ?

Ieleweke kwamba siwadharau hata kidogo wale walioshika dhamana hii pale ambapo matajiri, wasomi na watu wengine wenye majina walipoidharau na kuikataa. Ila kutokana na mabadiliko ya wakati ambapo sasa Tanzania ni sehemu tu kiuchumi katika ulimwengu mkubwa zaidi naona upo umuhimu wa kujitazama na kujipanga upya ili tuweze kuzikabili changamoto mbalimbali za maendeleo zinazotukabili.

Pengine kuna kosa la kiufundi lililofanyika katika ugawaji dhamana na maslahi yanayoendana na hili. HIvi anayestahili kulipwa mshahara mzuri ni kiongozi wa ngazi ya chini kabisa (ambaye anaweza kuibadili hali ya watu wake toka umaskini au daraja la tatu wakawa la pili au la kwanza) au kiongozi wa ngazi ya juu ambaye nadra kuwa na mawasiliano na wananchi huko waliko?

Ukweli ni kuwa viongozi wetu wa nyumba kumi, wenyeviti wa mitaa na makatibu kata wote elimu yao, uzoefu wao, uono wao na ufahamu wao wa dunia ya utandawazi bado uko chini kwa upande mmoja. Na kwa upande wa pili maslahi na motisha yao ya kuleta mabadiliko ya kimsingi katika jamii zao ni sawa na hamna au ni kidunchu mno. Hii haina tofauti na mameneja, makocha na viongozi wengine wa timu ya michezo kulipwa mara kumi au ishirini ya wachezaji halafu timu ikawa inadorora mwaka nenda, mwaka rudi -halafu unatafuta mchawi nje yenu !

Viongozi au watu wanaoitwa viongozi katika ngazi za chini kwenye nchi hii ni watu wasiolipwa mishahara; hawana elimu ya kutosha kuongoza na kuleta mabadiliko katika jamii; hawana ari, motisha wala moyo wa kufanya kazi; hawana ujuzi na uzoefu katika kazi wanazozifanya na wala hakuna taasisi iliyojipanga au kupangwa kuwafunza na kuwaendeleza.

Viongozi hao wa chini wengi ni masikini kiasi cha kutisha kiasi ambacho sio tu wana vishawishi vingi bali pia wanakuwa sio amana bali deni kwa taifa na hasa pale wageni toka nje ya eneo lao au nje ya nchi wanapokuja na kitita cha fedha na kuwashawishi zaidi. Au wanapotishwa na viongozi wa ngazi ya kitaifa hadi kuwadhulumu na kuwaonea watu wao wenyewe.

Hata tupate viongozi wa kitaifa ambao wote ni maprofesa lakini huku chini tuna watu wasiosoma, masikini na wenye ujuzi sawa na hamna katika masula ya uchumi, biashara, uwekezaji, ujasiriamli, menejimenti, usimamizi wa fedha, sheria na kadhalika nchi yetu haiwezi kamwe kuendelea.
Tutajenga kama mataifa mengine yaliyopotea kizazi cha viongozi wanaorithiwa na watoto wao mwaka nenda, mwaka rudi. Ni mwanzo wa kuwa na nchi ambayo itakubali na itaendelea kukubali uongozi mbovu kwa sababu mfumo uliopo hauna chachu wala changamoto inayoiwezesha kupata fikra mbadala na viongozi wenye misimamo na mitazamo mipya na inayobadilika na wakati.

Kazi zao nyingi hazina usaidizi wa aina yoyote ile ukiwa ule wa zana, fedha au rasilimali watu. Na kwa hiyo, kwa wakati mwingi ni sehemu ndogo ya yale yaliyostahili kuwa majukumu yao yanatekelezwa kikamilifu.

Wrengi wanajiona wanatumika zaidi kisiasa na baadhi yao wanaamini pengine kile walichostahili kulipwa huliwa na wale walio juu yao. Zaidi ya hilo mara chache sana maamuzi yana sauti katika masuala mbalimbali. Kwa hiyo huiona zaidi ni yoyo kuliko watu wenye sauti katika mambo mengi yanayowazunguka. Nafuu kwao huja wakati wa chaguzi kwani ndipo wanapoweza kupambanisha pande mbalimbali na kuzikamua angalau wapate maziwa ya watoto.

Huu ni wakati mzuri wa kujiuliza, hivi, kama viongozi wa ngazi za chini wangekuwa na elimu, maarifa na uono sawa na wale wa juu majimbo yetu ya uchaguzi yangelikuwa kama hivi yalivyo. Na, je ni mtaji kwa serikali kwa wananchi vijijini kuwa mbumbumbu wa faida za siasa za ushindani ? Na wabunge tunaowapata kwa mfumo huu wa sasa wangelikuwa ndio hao hao katika mazingira ambayo kuna wasomi kushinda wao katika ngazi za uongozi wa chini ?

Ni rahisi kuelewa kwa nini hakuna anayetaka kugombea nafasi za kuwa mjumbe wa nyumba kumi au balozi au diwani au mwenyekiti wa serikali ya mtaa. Kwa upande mwingine kila mtu anataka kugombea ubunge, uwakilishi na urais. Hata hao waliopo asilimia 80 ya muda wao hutumika kujitafutia riziki kwingineko na ni kama asilimia 20 tu ndiyo hutumika kuangalia mambo ya wananchi/serikali.

Kutokana na ukweli huu kwamba kuna mfumo na hali ambayo inasababisha watu watake kugombea ubunge, uwakilishi na urais lakini hakuna wanaotaka kugombea ubalozi wa mitaa au uenyekiti wa mtaa ni dhahiri kuwa ipo haja ya kuleta mapinduzi makubwa ya uongozi katika ngazi za chini ikiwa kama kweli tunataka tujikwamue na hali hii ya kuwa masikini wakubwa duniani. Na uongozi wowote (uwe wa chini au wa juu) lazima uwe ni kazi au tarafu inayolipwa kima mahsusi kinachowawezesha viongozi hao wote kujitoa kwa hali na mali kutimiza zaidi majukumu yao ya kikazi kuliko ya kibinafsi.

Tuanze na utafiti na ushauri

Ninapendekeza kuwa Chuo Kikuu cha Mzumbe kikishirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania chenye tawi karika kila mkoa waanze kwa utafiti na ushauri katika kila mkoa kuona ni namna gani tunavyoweza kuongeza hatua kwa hatua, ubora wa viongozi waliopo na wakati huo huo kuwashawishi watu wenye uwezo, elimu na ujuzi zaidi kukubali kuwa wajumbe wa nyumba kumi na viongozi wa serikali za mitaa. Bila kuwasahau madiwani wetu. Baada ya kazi za utafiti na ushauri yaanze mafunzo na uandaaji wa mipango ya urithishaji uongozi kwa namna ambayo kila mtaa, kila kata inapata kiongozi anayestahili kushika nafasi hiyo.

Ninaamini ya kwamba, masomo kama vile yale ya uchumi, uongozi( leadership) utawala (governance) , uangalizi wa fedha, menejimenti, sayansi ya jamii, usimamizi rasilimali watu, mipango, udhibiti, sayansi ya maamuzi na kadhalika hayatakosekana na yatatolewa kwa lugha mama ya Watanzania, yaani, Kiswahili.

Sio rahisi bila ya nafasi za uongozi katika ngazi za chini kushikwa na watu wenye ujuzi, elimu na uono mpana wa dunia hii ya utandawazi kwa watu wetu kuamka na kufanya kile kinachotakikana kama majibu yetu kwa mfumo wa uchumi, biashara na teknolojia unaogeuka kila kuchwao.

Mapinduzi ya uongozi Tanzania yataanza pale itakapogundulika kuwa nafasi hizo si za wanasesere au vibarakala(puppets) bali za watu muhimu mno katika kuikwamua Tanzania kutoka kwenye umaskini na wanaostahili kupewa ila nyenzo ili waweze kuhamasisha watu na jambo hilo likafanyika bila kusubiri ziara na misaada ya wakubwa toka makao makuu ya nchi yawayo.

No comments:

Post a Comment